advertise with us

ADVERTISE HERE

YANGA KUSAJILI MASHINE MPYA NI YULE ALIEWATOA SIMBA LIGI YA MABINGWA AFRIKA

YANGA inajipanga kufanya bonge la usajili wa nguvu ili kwendana na kasi yao , huku jina la Luís Miquissone wa UD Songo ya Msumbiji likiwa la kwanza kutua mezani kwa Mwenyekiti wa Wanajangwani hao, Dk. Mshindo Msolla, likifuatia la mkali wa Platinum ya Zimbabwe, Perfect Chikwende.

Wakati Miquissone akikumbukwa na wapenzi wa soka hapa nchini kwa bao lake la mpira wa adhabu aliloifunga Simba hivi karibuni katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na BINGWA, Dk. Msolla alisema kuwa pamoja na kuwa na kikosi kizuri, lakini wanadhani kuna umuhimu wa kusajili wachezaji mahiri zaidi wa kuamua matokeo ya mechi zao, kuanzia za Ligi Kuu Tanzania Bara hadi za kimataifa.
Alisema wanaamini kuna uwezekano wa kikosi chao kufika hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika hivyo kupata nafasi ya kukiongezea nguvu kikosi chao, akiahidi kutofanya kosa katika hilo.
“Wachezaji tulionao si wabaya sana, tatizo tulilonalo tumeingiza wachezaji wengi wapya, wanahitaji muda wa kukaa pamoja kwa muda mrefu…kwanza hata kwa timu ilivyo sasa, mwalimu Zahera (Mwinyi), amejitahidi sana,” alisema.
Hata hivyo, Dk. Msolla, alikiri: “Pamoja na hilo, tunahitaji kupata wachezaji wa kiwango cha juu zaidi wa kuamua matokeo…mchezaji kama yule wa UD Songo (Miquissone) ambaye shughuli yake sote tuliiona walipocheza na Simba. Ukiwa na wachezaji wawili au watatu kama wale, unakuwa na uhakika wa ushindi.”
Alipoulizwa iwapo Miquissone yupo katika mipango yao, Dk. Msolla alisema: “Ndiyo, kuna mtu analishughulikia hilo, lakini pia tunaendelea kuwafuatilia wengine wenye kiwango cha juu kutoka katika timu hizi zilizopo Ligi ya Mabingwa, tutaangalia wale watakaong’ara hatua za awali na raundi ya kwanza kabla ya kuingia makundi.”
Lakini wakati Dk. Msolla akimpigia hesabu kali Miquissone, ukweli ni kwamba itakuwa ni ngumu mno kwa Yanga kumpata nahodha huyo wa UD Songo kwani kwa sasa ni mali ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ikiwa imemsajili kwa mkataba wa miaka minne, ikimwacha aendelee kupata uzoefu ndani ya kikosi chake hicho.
Juu ya hilo, Dk. Msolla ameapa kuwa tayari kuvunja benki kumsajili mchezaji yeyote ili kukata kiu ya mashabiki wa klabu yao.
Vipi kuhusu Chikwende? Mchezaji huyo ambaye aliiongoza Platinum kushinda mabao 4-2 juzi dhidi ya UD Songo, tena wakiwa ugenini, inaweza isiwe rahisi kwa Yanga kumpata kwani timu yake hiyo imetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, mbele ya suala la fedha, hakuna kisichowezekana hivyo iwapo Yanga watakuwa tayari kuvunja benki, wanaweza kumpata na hivyo kukifanya kikosi chao kuwa moto wa kuotea mbali.
Chikwende raia wa Zimbabwe, ana umri wa miaka 26, akiwa ndiye injini ya Platinum katika kuzalisha mabao na kufunga pia.
Kikosi cha Yanga kimeonekana kukosa makali ya kucheka na nyavu hadi sasa washambuliaji wake, wakiwa wameshindwa kufunga mabao zaidi ya mawili katika mechi za mashindano.
Washambuliaji wanaotegemewa na Yanga kwa sasa ni Juma Balinya, Sadney Urikhob, Patrick Sibomana, Issa Bigirimana, Maybin Kalengo, Mrisho Ngassa na Deus Kaseke. 

Post a Comment

0 Comments